Sunday, 28 September 2014

Siri ya misingi ya upendo wa kweli





Siri ya misingi ya upendo wa   kweli

MWL. MICHAEL L. KIHWELE
Zaburi 18:32-33” Mungu ndiye anijaliaye nguvu kila upande; ndiye anayeifanya salama njia yangu. Ameiimaraisha miguu yangu kama ya paa, na kuniweka salama juu ya vilele.

Naomba Watanzania wenzangu na Afrika Mashariki pamoja Africa nzima na dunia yote kwa lugha zote mnisaidie kutangaza habari hii ili tupone. Let us talk in one voice to make the world peace and love.

Biblia inasema nini?
Neno la  mwisho ni hili, muwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitivu, wanyenyekevu, watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hiyo ndiyo mlioitiwa ili mrithi Baraka. 1 Petro 3:8-9

Maana kwa jinsi Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanae wa pekee afe msalabani ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele. Yohana 3:6
 Zaburi 19:7 “Sheria ya Bwana ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya; shuhuda za Bwana ni za kweli, huwapa hekima wasio na makuu.
Yohana16:6 “Yesu akamwambia, mimi ndimi njia ya kweli na uzima, mtu hawezi kwenda kwa baba bila kupitia kwangu”

Waebrania 13: 1 “Upendo wa ndugu na uzidi kudumu msisahau kuwafadhiri wageni maana kwa njia kama hii wengi wamewapokea malaika pasipo kujua


Shukrani
 Awali ya yote namshukuru Mungu muumba wa mbingu na dunia pamoja na vyote vilivyomo ndani yake. Pili nawashukuru wazazi wangu kwa kukubali kunilea katika maadili ambayo hata hivi leo nasubutu kuandika kitabu hiki: hizi zote ni matunda ya malezi yao. Tatu napenda kutanguliza shukrani zangu za dhati ziende kwa Bw. Emmanuel Lucas Kihwele ambaye ni kaka yangu wa kwanza pia ndiye mlezi wangu kielimu niliyo nayo pengine sikustahili kuipata, ni jitihada zake. Naomba Mungu ambariki yeye na mke wake. Pia namshukuru mke wangu kipenzi Magreth Mathias Nkwabi, kwa usikivu na uvumilivu alionao katika kufanikisha uandishi wa kitabu hiki.
Nitakuwa mchoyo wa shukrani kama nitamwacha nyuma rafiki yangu wa damu, Mwl Salehe Amiri Mtamike na mke wake Witness Mussa Nakembetwa kwa ushirikiano na upendo walionionesha pindi naandika kitabu hiki na maisha ya kila siku tunaishi kiujumla; naomba Mungu azidi kudumisha ushirikiano wetu
Mwisho kabisa napenda kurudisha shukrani zangu za pekee kwa ndugu yangu Mch. Madson Lukas Kihwele kwa kunifundisha upendo pale ninapokata tamaa. Pia ndugu zangu wote Nawapongeza kwa kunifundisha mwenendo mzuri wenye maadili ya Kiafrika, Mungu mwenyezi awabariki wote.

Nini maana ya upendo?
Upendo ni msukumo wa asili ,ambao hatuwezi  kuulazimisha kuwa nao, lakinini kila mmoja anahitaji kuwa nao au ahitaji kupoteza hisia zake. Japokuwa watu wengi wanaamini kuwa upendo ni ufahamu ambao kimiujiza humfanya mtu kuonekana yuko sawa na watu wengi kumwamini na kutokuwa na mashaka naye.
Kulingana na historia ya wanafalsafa mbalimbali duniani, tangu miaka 400 iliyopita ya historia ya kitaalamu duniani,kama ilivyo nakiliwa na mwanafalsafa Maria Popova
    “Upendo hauna kitu chochote cha kufanya juu ya kile
      Utarajiacho kupata -ila tu katika yale utarajiayo
      Kutoa - ambayo ni kila kitu.”
Upendo hauangalii mema mangapi umetendewa, bali mazuri mangapi umeyatenda au unatarajia kutenda katika jamii yako, ukizingatia hayo moyoni mwako,utaamsha hisia ya upendo na huruma nafsini mwako katika kujali na kusaidia maisha ya watu wengine pamoja na kulinda haki za watu na kuheshimu thamani zao.
Kwahiyo upendo unaweza kumbadilisha mtu kama vile mzazi awezavyo kubadili mwenendo wa mwanae. Hakuna mahusiano ya kibinadamu katika jamii yoyote ile duniani isipokuwa kwa njia ya upendo.
Kwa hiyo watu wawili au zaidi wanapotofautiana kauli, hisia au mtazamo huwapelekea kutokuelewana, na matokeo ya kutokuelewana ni chuki, husuda, kiburi, hasira na visasi na upendo kutoweka. Hari hii inaweza kuanza baina ya mtu na mtu, familiya na familiya, koo moja na koo nyingine, pahala pa kazi, chama kimoja na chama kingine cha siasa, au nchi moja na nchi nyingine zilizopishana kisiasa. Upendo ukitoweka hauna mbadala yake, Upendo ukitawala katika jamii yoyote duniani huleta amani baina ya wanajamii.
Shakespeare katika simulizi lake lenye jina la “A mid summer Night’s Dream”:
Ameeleza kuwa
      “Upendo hauonekani kwa macho, bali nafsini kwa mtu”.
Kumbe upendo huanza moyoni mwa mtu, na kisha huambatana na matendo yake ya nje pamoja na kauli. Kwasababu kimtokacho mtu ndivyo alivyo nafsini mwake. Ukisoma katika kitabu kiatakatifu Biblia:
         Mithali 23: 7a- Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo
Kwani upendo hauhesabu makosa, haujivuni, hautakabali bali huvumilia. Lakini roho isiyo na upendo haina uvumilivu, imejawa na kiburi, kisasi, husuda, hasira na ubinafsi. Bila kusahau majivuno na kujiinua.

Nini chanzo cha Upendo?
Chanzo cha upendo alionao mtu ni kazi kuuelezea, kutegemeana na mtazamo wa mtu na jinsi alivyo moyoni mwake, pia namna ya moyo wa mtu unavyoridhika katika kutendewa, kutenda na kuthaminiwa na jamii anayoishi nayo. Kwasababu kila mtu anaweza kueleza chanzo cha upendo kulingana na hisia zake zilizo moyoni mwake. Mtu aliye na hisia za mapenzi huweza  kusema upendo chanzo chake ni kumjali mwenzi wako, au kutimiza ndoto za mwenzi wako kulingana na makubaliano  yao. Aidha kwa watu walio na hisia za maendeleo, huweza kusema kuwa upendo chanzo chake ni kutokuwa na husuda na tamaa mbaya kwa maendeleo ya mtu mwingine. Kujali na kuheshimu maisha ya watu wengine bila kujali tofauti za kiuchumi, kisiasa na kidini.
Lakini mwanafalsafa mmoja, James Baldwin (1948- 1985) katika simulizi lenye jina la “The Price of the Ticket”. Amesema kama ifuatavyo juu ya upendo
  “Upendo hauna mwanzo wala mwisho kwa namna tunavyo
    fikili ulivyo, lakini upendo ni kupambana, upendo ni vita.
    Upendo unakuwa kadiri mtu akuavyo.”

Hivyo basi upendo ni tabia ambayo mtu amezaliwa nayo, na kisha kadiri akuavyo na upendo ulio moyoni mwake ukuwa na kutoa matunda yake. Mtu aliye na upendo moyoni mwake kila wakati huwa na furaha na kila mtu, hahesabii makosa ni mwenye roho ya kusamehe, asiyekumbuka mabaya na mwenye kuhesabia jema moja kwa mabaya mia moja, mvumilivu, hasiye na haraka katika kutenda kwa msukumo wa hasira. Mtu hasiye mbinafsi wa haki na hasiye na dharau katika mambo madogo yanayowapata watu wengine, hususani matatizo ya kiafya, kiuchumi na kielimu, kwasababu kwa asili yake hakuna tatizo lilo dogo na kufurahiwa., 
 Louis de Bazac- amesema hivi
  “Kadiri mtu ahukumuvyo, ndivyo kadiri upendo upunguavyo”
Upendo ni vigumu sana kuuelewa, lakini ni zaidi ya jinsi ujuavyo asili ya kitu Fulani. Ukimfikiria mtu katika mambo mabaya wakati wote hakika hautampenda. Jaribu sana kumfikiria mtu katika mtazamo chanya, hali hii mara zote inaimarisha umoja wa watu walio na utamaduni mmoja na utaratibu wa jamii moja, unaongozwa na kanuni moja ya maisha.

              Je, upendo huleta haki?
Mtu akiwa na upendo yuko radhi kafa kwa ajili ya mtu mwema, lakini kwa mwanadamu wa sasa hakuna hata mtu mmoja ambaye yuko tayari kufa kwa ajili ya mwenye haki. Ndiyo kwanza wenye haki wanafungwa, wananyongwa na kuumizwa hata kufa kwa sababu upendo umegeuzwa kwa kutegemea kitu apokeacho mtu. Madhara ya upendo wa namana hiyo kumezaa rushwa na ufisadi. Ukisoma katika biblia takatifu katika kitabu cha Warumi 5:7 utaona kuwa mwanadamu ni mtu wa kujipenda mwenyewe. Huthamini sana vya kwake na nafsi yake kuliko nafsi ya mwingine. Hayuko mtu aliyetayari kutetea haki ya mtu mwingine, kila mtu huona kuwa ana haki kuliko mwingine hata kama hakustahili haki. Na ndiyo maana watu wanawaua wenzao kwa ajili ya kuzitosheleza nafsi zao. Ona mauaji ya vikongwe kule Shinyanga Tanzania, ona mauaji ya maalubino kwa ajili ya kupata utajiri, yote hii ni kwa sababu ya kutothamini haki za watu wengine za kuishi duniani. Majambazi nao hupora na kuua watu kwa ajili ya kujipenda wenyewe, wanasiasa mbalimbali huanzisha mapigano kwa kutumia silaha nzito kwa ajili ya kutimiza haja ya nafsi zao za kuwa viongozi bila kuthamini maisha ya watu wengine. Kumbe haki hutafutwa kwa njia ya mazungumzo.
           Warumi 5:7- “Kwakuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu
                                 mwenye haki”, lakini yawezekana mtu 
                                 kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema.

Upendo wa namna hii tunauita ni upendo wa kiungwana,uliozaidi ya kibinadamu. Yaani ni upendo wa Mungu mwenyewe ambao katika Yesu kristo  tumepokea upatanisho wa mioyo yetu, ambao kwa ajili yetu kristo alikufa ili sisi tuliokuwa adui wenye dhambi tupatanishwe na Mungu kwa njia ya mauti   yake. Huu ni upendo upitao fadhiri za kibinadamu, kwa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya uhai wa  watu wengine wakosaji wenye dhambi.
           Warumi 5:8 - Bali Mungu aonesha pendo lake yeye
                                 mwenyewe kwetu sisi, kristo alikufa kwa ajili
                                 yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi.

Mtu akiwa na upendo moyoni ni jambo jema. Hatakubali mwenye haki aonewe, atafanya kila linalowezekana kumnusuru mwenye haki. Kama mama ahangaikiavyo kumnusuru mwanae pindi awapo mgonjwa au mwenye njaa kwa kuwa mama ni mtu mwenye upendo sana kwa mwanae. Japo baadhi ya wanawake wanawaua wana wao mara baada ya kuwazaa, au kuwatupa porini au majalalani kwa sababu ya ugumu wa maisha au matatizo ya kifamilia ambayo huwapelekea katika mfadhaiko wa mawazo na kisha kupelekea mjengeko wa roho za kikatili badala ya upendo moyoni mwao. Lakini kovu  la matendo kama hayo hayafutiki mpaka mwisho wa uhai wao, kwa sababu walivyoumbwa ni kuwa na upendo.
   Laiti kama wanaume tungaliimarisha upendo kwa dada, mama na wake zetu, watoto wa mitaani wasingalikuwepo, wala mauaji ya kikatili duniani yangepungua. Kwa sababu vitokeapo vita wanaotaabika sana ni wanawake na watoto, kwanini? Kwa sababu mama hayuko tayari kukimbia kuwaacha watoto wake, wanaune wanawatenda vibaya wanawake na watoto wasio na hatia. Kwa kuwa upendo haupo ndani yao. Mimi ni mwafrika, naweza kuthubutu kusema jamii ya kiafrika tumepungukiwa na upendo au hatuna upendo kabisa, kwasababu bara zima la Afrika tunaangalia watu wachache wenye roho zisizo na upendo kuwafanyia ukatili watu wengi wasio na hatia kuangamia. Pengine baadhi ya nchi kupeleka majeshi yao kupora mali na kuwasaidia wenye roho za ukatili kuua wengine pasipo kujali. Japo kuna baadhi ya nchi barani Afrika zilizo mstari wa mbele kusaidia kurudisha  mshikamano baina ya nchi zilizo na vita, kwa mfano;Tanzania, Uganda Kenya na Rwanda hizi ni baadhi ya nchi chache za Afrika zilizo kifua mbele kuwahurumia waafrika wengine kwa kupeleka majeshi yao kulinda amani. Japo zingine zipo pia za namna hiyohiyo Afrika.
Biblia takatifu inatuonya katika katabu kile cha waraka wa Paulo mtume kwa Wathesalonike wa pili 3:11-15
 
 “Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu,hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo,watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. Lakini ninyi ndugu msikate tamaa katika kutenda mema. Lakini ikiwa mtu awaye yote hashiriki neno letu la waraka huu, jihadharinini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari: Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.”
Wanadamu! Mungu wetu aketiye mahali pa juu sana ametuumba tuishi katika hali ya utaratibu, kufanya kazi kwa bidii, uvumilivu, kuonyana na upendo. Utaratibu huu wa kufuatilia mambo na kufanya kazi za watu wengine kwa manufaa yao na siasa za kiuchumi wa chi zao na kuoneana, huo sio utaratibu utokao kwa Mungu Yule aliye tuumba bali unatoka kwa miungu ya kishetani ambao ndani yake kumejaa uharibifu mkubwa.
Ni fursa nyingine kwa watu wa Afrika kukataa kata kata fursa ya vita kama suluhu ya matatizo yetu, badala yake tujikite katika sera na mikakati inayopania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho wa kweli kati ya watu. Maisha ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu, yanapaswa kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake. ( kauli ya baraza la maaskofu katoliki Afrika)
Mtume Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa Timotheo, amasema
  ” Wala wasianagalie hadithi na nasaba zisizo na ukomo, ziletazo maswali wala si madaraka ya Mungu yaliyo katika imani; basi ufanye hivyo. Walakini mwisho wa agizo hilo ni upendo utokao katika moyo safi na dhamira njema, na imani isiyo na unafiki. Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili; Wapenda kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo yale wayanenaye kwa uthabiti.” 1Timotheo 1:4-6
Kutokana na maneno hayo matakatifu kama yalivyo nenwa na mtume Paulo kwa Timotheo. Kiongozi lazima awe na upendo utokao katika moyo safi na dhamira njema. Watu waliokosa upendo na moyo safi hugeukia katika ukatili, mauaji, utekaji nyara, uchawi na uvunjaji wa sheria, yaani kupotosha hukumu. Asiwepo katika pahala fulani kiongozi hasiye na dhamira njema, kama akiwepo lazima pahara pale amani ikosekane.
Amani ikikosekana katika jamii yoyote ile duniani, upendo hutoweka na upendo ukitoweka katika jamii,basi jamii hiyo haitatawalika.
Biblia inaendelea kutufundisha kwa kusema kwamba
       “Lakini twajua ya kuwa sheria ni njema,
        kama mtu akiitumia kwa njia iliyo halali” (1 Timotheo 1:8)
Unapokuwa kiongozi au msimamizi wa sheria, Vitabu vitakatifu tunavyoviamini sisi waamini wa dini mbalimbali duniani vinatufundisha kuwa; watu waasi, wasio wataratibu sheria na iwabane. Usiruhusu watu kudhurumu haki ya watu wema. Usiseme uongo wala usiibe mali ya umma. Hivyo vyote ni ishara ya kutokuwa na upendo, usipende pesa mbele kabla ya haki, ukifanya hivyo unaruhusu mianya ya rushwa. Na mianya ya rushwa ikitawala itawagawa watu unaowaongoza, kutakuwa na tabaka la watu wenye kipato na tabaka la wanyonge wasio na kipato cha kutoa kitu chochote ili wasikilizwe na kutatuliwa kelo na shida zao.
Matokeo ya hayo yote watu watakosa  uzalendo na nchi yao, viongozi wao, vyombo vya sheria na haki, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama na kujenga chuki na serikali yao. Chuki ikitawala amani hutoweka, na amani ikitoweka upendo nao hudhoofika mioyoni mwa watu, hatima ya yote mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, maandamano na migomo katika taasisi za serikali na kwa jamii unayoitawala kwa ujumla, pamoja na ubabaishaji mwingi katika utoaji wa huduma za kijamii.

Raisi wa awamu ya nne katika utawala wa Tanzania baada ya uhuru Dr. Jakaya M. Kikwete, amewahi kusema katika moja ya hotuba yake redioni (mwaka 2014) kwamba:
             “ Amani na upendo vikitoweka havina mbadala yake
                isipokuwa mafarakano na mauaji”
Kiongozi mzuri ni Yule anayelinda na kusimamia vizuri katiba ya jamii yake, kwa kuwa katiba ni makubaliano ya wengi yaliyofanywa kwa mahojiano ya pamoja yanayotambulika kisheria.
Wanasheria wahukumu kwa haki kwa kulinda amani na upendo wa nchi yao. Kadhalika na askari nao walinde rasrimali na uhuru wa watu walio katika nchi yao.
 Na wewe ulioajiriwa unatakiwa kuwa na upendo wa kuhudumia wengine na kuridhika katika kile unachopata, kwani kumbuka kuna wengine hawana hicho unachopata wewe, japo wanaishi katika jamii unayoishi wewe na wanahaki sawa kama wewe, lakini hutegemea shughuli zao za kila siku. Mtu yeyote akikosa kuzingatia hayo basi huyo amekosa upendo, kwani upendo huimarisha uwajibikaji katika yale utarajiayo kuyatenda.

Je Upendo huleta viongozi bora?
Ninyi ni kama wanadamu vijana, watoto na wazee wa urithi ulio nadra, ni watoto halisi wa Mungu mmezaliwa katika nyakati hizi maalumu za kihistoria ya dunia kwa kusudi takatifu la Mungu. Wakati na zama hizi za sasa maadili ya kitabia na kidini ya jamii yanaonekana kudhoofika katika jamii nyingi duniani kote. Aidha mabadiliko na maendeleo ya kisiasa yanaendelea kupamba moto, pia mageuzi ya kisayansi na tekenolojia yamekuwa makubwa pasipo kifani. Dunia imefanywa kuwa kama kijiji, hivyo na ufahamu wa watu umeongezeka. Hivyo basi dunia imekuwa pahala pasipo tawalika kiurahisi. Kiongozi yeyote wa zama hizi za utandawazi aanatakiwa kuwa na upendo, elimu na maarifa pamoja na maadili mema.
Biblia inasema:
   “Angalieni nimemweka kuwa shahidi kwa kabila za watu;
     kuwa   kiongozi na jemadari kwa kabila za watu” (Isaya 55:4)
Kumbe uongozi umewekwa na Mungu mwenyezi, huotoa mwongozo wenye nguvu ya kutatua matatizo ya jamii kwa mafanikio. Ukiona kiongozi yeyote duniani antoa mwongozo wenye kuwadhuru watu anaowaongoza basi ujue amepungukiwa na upendo au pengine hana upendo kabisa.
Katika kitabu ch Warumi 12:7-10, Biblia inaelezea kwamba:
 “Ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake. Mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukarimu kwa moyo mweupe, mwenye kusimamia kwabidii mwenye kurehemu, kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki, lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema”.
Kiongozi bora ni yule mwenye uwezo wa kutumia mamlaka aliyonayo vizuri, katika kukemea, kuonya na kutoa maamuzi sahihi yasiyoweza kufukuza amani bali yenye kuimarisha mshikamano, amani na upendo miongoni mwa watu anaowaongoza. Ni mtu mwenye kulinda kauli ya midomo yake na hasiye mwepesi katika kunena bali aliye mvumilivu mwenye moyo safi usio na unafiki, mpenda haki na mwaminifu.
Wanafalsafa mbalimbali duniani wa uongozi, wanasema kiongozi bora anaweza kuleta mabadiliko na mageuzi ya utendaji katika mfumo wa kiutendaji wa utoaji wa huduma ya jamii, hivyo kiongozi bora anpaswa kuwa na huruma kwa wafanyakazi wanaotoa huduma kwa jamii, ili watumishi hao wawe na upendo na kazi zao, kisha kuongoza bidii katika kazi zao kwa moyo. Viongozi wanapaswa kutenda kama vile wangependa wafuasi wao watende, kwa kufanya hivo watakuwa wamegusa tafsiri ya neno upendo.

Upendo huokoa Taifa bali Amani huinua uchumi wa Taifa
Watu wakiwa na upendo pahala popote duniani au taifa lolote lile ulimwenguni, Taifa hilo huwa na amani. Na amani ikiwepo basi katika pahala hapo huwa na maendeleo ya kidemokrasia na uchumi. Mimi kama Mtanzania mzawa naona hamasa sana kuishawishi jamii ya Kitanzania kuulinda mshikamano tulionao ambao tumepewa kama dhamana ya upendo tulionao, ambao kwa sasa umetufanya tudumu katika umoja tulionao na kutuwezesha katika mshikamano tunaodumu nao hata hivi leo, ulioletwa na waasisi wetu wawili ambao ni hayati Mwl. J.K Nyerere pamoja na A.A Karume. Hili ni jambo la kupokelewa kwa mikono miwili na kulienzi. Mshikamano ni chanzo cha umoja wetu na uzalendo wa Watanzania, nawashawishi vijana wa Kitanzania kuwa na uzalendo wa nchi yetu. Tusikubali kuwa madaraja na ngazi katika kulididimiza taifa letu wenyewe. Uchumi wa nchi hii utaletwa na kuinuliwa kwa umoja na uzalendo wa Watanzania wote, bila kujali wewe ni nani, unaelimu gani? Unacheo gani? Umesomea kada gani? Muumini wa dini gani au unatoka katika kabila lipi. Tukisimama katika muungano wa umoja wetu, hayupo wa kutugombanisha, umoja ni silaha kubwa ya ushindi wenye tija kwa maendeleo ya kila Mtanzania. Tuthamini rasrimali za taifa letu Tanzania, tuwaheshimu waliotutangulia kiumri, tuwe wasikivu tunapoelimishwa na watu waliokuwa mbele yetu kidesturi, elimu hisiwe kama silaha ya kukwamisha maendeleo ya shughuli za kijamii.
Wasomi wawe mstari wa mbele katika kuisaidia jamii kutatua migogoro itokanayo na mabadiliko ya kitekinolojia, siasa na kiuchumi duniani. Kwasababu ni lahisi kwa wasomi kujua wapi tuliko toka, tulipo na tunako kwenda, tusipuuze, tuwe na upendo wa ustawi wa taifa letu. Ukombozi wa taifa hili umo mikononi mwa Watanzania wote, tusipodumisha amani na upendo tutakuwa wakimbizi katika taifa letu. Hii ni kauli ya mama Maria J.K Nyerere katika moja ya hotuba zake redioni.
Watanzania tunamengi ya kujifunza kutoka kwa aliyekuwa waziri Mkuu wa tatu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine kwa jinsi alivyokuwa kielelezo cha kupigania wanyonge (Waziri Mkuu Mizengo Pinda amenena kauli hiyo siku ya Jumanne, Aprili, 12, 2011).” Marehemu Sokoine atakumbukwa kwa mengi ambayo tukiyaongelea hatutaweza kuyamaliza, tunamkumbuka mtu ambaye kwetu sisi Watanzania ni kielelezo bora cha utumishi, kujituma, upendo na kupenda haki na kielelezo cha kumcha na kumtumikia Mungu.
Askofu wa jimbo katoliki Dodoma, Mhashamu Askofu Gervas John Nyaisonga katika moja ya ibada zake, alisema kumbukumbu ya kifo cha Sokoine kiwakumbushe Watanzania ni nini cha kujifunza kutoka kwake katika kuenzi tunu alizoacha. Alisema alikuwa mtu wa kipekee kwani alijitolea kukatwa 50% ya mshahara wake ili kuchangia katika mfuko wa nguvu kazi ili wananchi wasio na uwezo wa kukopa benki waweze kupata mikopo kutoka katika mfuko huo”. Huu ni upendo wa ajabu kuwepo katika taifa letu uliofanywa na hayati Edward Moringe Sokoine, ni tunu yenye kuinua maendeleo ya watu wengine.
Pengine naweza kusema hawapo tena watu wenye mapenzi mema na taifa letu kama Sokoine, kama wapo basi kunawalakini kwanini hawajitokezi? Watu twapaswa kufahamu kuwa umoja wetu ndio utakao weza kutufanya tuyaenzi hayo kama tutamwamini Mungu wa kweli aliye na huruma na pendo kwa watu aliowaumba. Tanzania tunakila sababu ya kuendelea lakini kama tutakuwa na uzalendo na taifa letu, kwani mti wenye matunda mazuri hauishi kupigwa mawe, tuchukue tahadhari katika kukwepa mawe tutashinda uwezo tunao.

Historia ya upendo wa mtu huanza toka katika familiya yake?.
Nakumbuka mimi ningalimdogo mwenye umri wa miaka tisa, siku moja nilipokuwa naumwa, mama yangu alinipeleka katika Hospital ya mtakatifu Francis Iliopo mjini Ifakara kutibiwa; tulipoingia kwenye chumba cha daktari, yule daktari alimfukuza mama kwa kebei kwamba hakuvaa mavazi mazuri, mama hakukubali kutoka kwasababu alikuwa ananihurumia mwanae kwa kuwa nilikuwa naumwa sana, na kiukweli wazazi wangu wote baba na mama walinipenda sana. Kiujumla sikukubaliana na maneno ya daktari, nilimwambia mama twende nyumbani mimi ni mzima japo nilikuwa naumwa sana, Kisha baba alinibeba mgongoni kama mtoto mchanga,hapo ulikuwa mhimili wa kuwapenda wazazi wangu na kuwasikiliza kwa kila jambo. Niligundua wazazi wangu walikubali aibu kwaajili yangu na ndugu zangu. Huo ulikuwa mwanzo wa upendo hata kwa watu wengine wenye shida hasa wenye kipato duni na wasio na elimu.
Watu wengi wakifanikiwa huwa wanaangukia kuwasahau wazazi wao na kuwadharau kana kwamba hawakuzaliwa na kulelewa nao. Ninao mfano mzuri kwa baadhi ya watu wakotayari kuwasaidia watu wengine ambao wanaowakubali na kupewa sifa kwamba wanahuruma na busara lakini wazazi wao hawana chakula au mahitaji muhimu. Je huo ni upendo? Au ni ushetani! Mungu wetu hakutuagiza hivyo bali amesema”Waheshimu Baba na mama yako ili siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana Mungu wako”.(Kutoka 20:2-17))
Tuwe na upendo kwa wazazi wetu, tukiwapenda tutawahurumia, na wala hatuta wasema vibaya au kuwasema kwamba wanajidekeza, tukumbuke wote tunaelekea uzeeni na katika hali walionayo, nawe utafikia, hakuna atakaye kwepa labda kwa mpango wa Mungu.
Lakini katika imani ya Kikristo Biblia inatufundisha kwamba ni wajibu wa wazazi kuwaheshimu na kuwatunza watoto wao katika misingi ya imani ya Kikristo, kama utakosa kuwatunza katika imani uliyozaliwanayo utawajibika na maisha yake. Waefeso 6: 4 “Nanyi kina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo.” Wazazi mkiwalea watoto wenu kwa upendo na mshikamano nao watadumu katika mshikamano huo huo katika kuwakumbuka siku za usoni pindi mkiishiwa nguvu za kujitafutia ninyi wenyewe katika hali ya uzee. Mimi nawapenda wazazi wangu wewe je?......
Ninawatakieni ninyi ndugu amani, upendo na amani  kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.” Waefeso 6: 23
Mwisho nawashawishi ndugu zangu tudumu katika pendo la kweli kama vile Mungu alivyo tupenda kwanza. Waebrania 13: 1 “Upendo wa ndugu na uzidi kudumu msisahau kuwafadhiri wageni

No comments: